Wednesday, August 8, 2012

MKAPA NA SIRI ZA FREEMASON


                             Benjamin Mkapa akiwa na Sir Andy Chande mwaka 1989.
                                                                    Mwaka 2002
                                                                         Mwaka 2003
                                                                       Mwaka 2003
                                                                Mwaka 2003

Na Elvan Stambuli
RAIS Mstaafu wa Tanzania, Benjamin Mkapa anaongozwa kwa kualikwa katika hafla mbalimbali zinazofanywa na jamii ya siri (secret society) ya Freemasons, hali inayoonesha kuwa huenda ana siri nyingi za taasisi hiyo, Uwazi limegundua.

Kwa mujibu wa mtandao wa kiongozi wa muda mrefu wa jamii hiyo, Jayantilal Kashavji Chande almaarufu Sir Andy Chande, picha nyingi za Mkapa zimewekwa katika mtandao huo na kuelezwa kile alichokuwa akifanya akiwa na kinara huyo wa Freemasons Afrika Mashariki.

MIAKA 100 YA FREEMASONS
Katika sherehe ya jamii hiyo ya kutimiza miaka 100 tangu waingie Afrika Mashariki iliyofanyika jijini Dar es Salaam Oktoba 9, 2004, Mkapa alialikwa na kuwa mgeni rasmi na sherehe hiyo ilifanywa kwa siri kubwa.

Gazeti hili limegundua kuwa Sir Andy Chande katika mahojiano yake na mwandishi mkongwe nchini, Ernest C. Ambali aliyekuwa akiandikia Gazeti la The Guardian, lililokuwa mitaani Oktoba 8, 2004 hakueleza mahali patakapofanyika sherehe hizo jijini Dar es Salaam lakini alitaja waziwazi kuwa mgeni rasmi angekuwa Rais (wakati huo) Benjamin Mkapa ambaye angefuatana na mkewe mama Anna Mkapa.

Hata hivyo, wakati anasimikwa Chaim Henry Gehl kuwa kiongozi wa Freemasons Israel, ilitajwa kuwa sherehe hizo zingefanyika katika Hoteli ya Royal Palm jijini Dar es Salaam ambapo wageni 350 walihudhuria.

MKAPA, SIR CHANDE UGANDA
Mkapa ameonekana katika picha akiwa na Sir Chande nchini Uganda walipotembelea Kiwanda cha Sukari cha Kakira wakati huo akiwa madarakani mwaka 2005. Haikuelezwa kwa nini walitembelea kiwanda hicho.

Sir Andy Chande katika kudhihirisha kuwa ni marafiki na Mkapa, alimpa nafasi katika kitabu chake kuandika utangulizi ambapo rais huyo mstaafu amesema kazi anazofanya mfuasi huyo wa Freemason kwa jamii ni nzuri.

Aidha, Mkapa amebainisha kuwa mara baada ya kufahamiana na mzee Chande, alimteua kuwa mjumbe wa bodi ya Shule ya Shaaban Robert jijini Dar es Salaam na kufanya naye kazi kwa karibu na ndipo alipoelewa zaidi shughuli za Freemasons ambazo ni za kusaidia jamii.
“Mkapa amekuwa akihudhuria hafla nyingi za Freemasons tangu akiwa Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Tanzania wakati wa utawala wa Mwalimu Nyerere,” alisema Mnajimu Maalim Hassan Yahya Hussein aliyehojiwa na gazeti hili.

Aliongeza kuwa shughuli za Freemasons nyingi huwa ni za kijamii na zinafahamika na karibu viongozi wote wa kitaifa waliopo madarakani na hata wale ambao waliongoza nchi.
“Kama kuna siri, basi Mkapa atakuwa anajua maana amekuwa karibu na Sir Andy Chande kwa muda mrefu, tangu enzi za Mwalimu Nyerere” alisema.
Katika mtandao huo, kiongozi wa pili ambaye anaonekana kuhudhuria hafla za jamii hiyo ni rais wa awamu ya pili, Mzee Ally Hassani Mwinyi akifuatiwa na Rais Jakaya Kikwete na hata aliyekuwa Waziri Mkuu, Frederick Sumaye.

MWALIMU NYERERE
Mwalimu Julius Nyerere naye ana picha mbalimbali mtandaoni humo akiwa na Sir Andy Chande na alikuwa akifuatana na Mkapa katika shughuli za kiserikali kwani imeelezwa kuwa kigogo huyo wa Freemasons alikuwa akiaminiwa sana na baba wa taifa kiasi cha kumfanya kuwa mwenyekiti wa bodi mbalimbali za mashirika ya umma aliyoyaongoza vyema.
Miongoni mwa bodi alizozisimamia kwa umakini mkubwa ni Shirika la Reli Tanzania (TRC) na Shirika la Usagaji la Taifa (NMC), mashirika ambayo baada ya uongozi wake yalizorota na hatimaye kufa. Sir Andy Chande pia amewahi kuwa Mwenyekiti wa Bodi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania.

Gazeti la UWAZI hivi karibuni lilimtafuta Sir Andy Chande kwa njia ya simu ili kuhojiana naye lakini mmoja wa wasaidizi wake, Ramji Suryakanti alisema kiongozi huyo amekwenda nchini India kwa ajili ya kupata matibabu.


 Source:Globalpublisher
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...