WAKATI kukiwa na taarifa kwamba maofisa wa Shirika la Upelelezi
la Marekani (FBI) wametua nchini kwa ajili ya kufanya upelelezi wa
mauaji ya Padri Evarist Mushi, Jeshi la Polisi limetangaza dau la Sh10
milioni kwa atakayefichua aliyemuua padri huyo.
Padri Mushi aliuawa kwa kupigwa risasi Jumapili
iliyopita wakati akienda kuongoza ibada katika Kanisa la Mtakatifu
Teresia lililopo Beit el Ras nje kidogo ya mji wa Zanzibar, ambapo
inadaiwa kuwa waliomuua walikuwa wamepanda pikipiki aina ya Vespa na
walimfyatulia padri huyo risasi tatu akiwa ndani la gari yake.
Wakati polisi wakitangaza dau hilo, Sheikh Ali
Khamis Ali (65) mkazi wa Kitope Kaskazini Unguja, aliuawa jana kwa
kukatwa mapanga mjini Zanzibar, baada ya wezi kuvamia shambani kwake.
Habari za kuaminika zilizopatikana juzi zinaeleza
kuwa maofisa hao wa FBI, wako nchini na tayari na wamekutana na baadhi
ya viongozi wa Serikali kwa ajili ya kuanza kazi hiyo.
Chanzo chetu cha habari kimeeleza kuwa maofisa hao
walikutana na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi kwa
ajili ya kuangalia ni namna gani watafanya shughuli zao katika
upelelezi huo.
Pamoja na ushiriki FBI, taarifa zinaeleza kuwa
maofisa wa Serikali ya Tanzania wamezungumza na taasisi za upelelezi za
nchi tano, ili kuongeza nguvu katika upelelezi huo.
Taasisi nyingine inayotajwa kuwa huenda ikashiriki
katika uchunguzi huo ni Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai ya
Uingereza (Scotland Yard).
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Pereira Ame Silima
alilithibitishia gazeti hili kwamba Serikali imeanza kufanya mazungumzo
na mashirika mbalimbali ya upelelezi duniani kwa ajili ya kushirikiana
nayo kuchunguza mauaji ya Padri Mushi, lakini akasema kuwa ni mapema mno
kuyataja.
“Tumefuata maagizo aliyotoa Rais Kikwete kwamba
tushirikishe mataifa mbalimbali kuchunguza mauaji yaliyotokea Zanzibar,
siwezi kutaja kwa majina, ila tayari tumeanza kuzungumza na nchi
mbalimbali,” alisema Silima.
Akizungumza mjini Zanzibar jana, Kamishna wa
Polisi visiwani humo, Mussa Ali Mussa alisema kuwa hadi sasa hakuna mtu
aliyefikishwa mahakamani kuhusiana na tukio hilo la mauaji.
“Hakuna aliyefikishwa mahakamani, lakini wapo watu
ambao wamekamatwa wakihusishwa na tukio hili na tunaendelea kuwahoji,
wengine tunawaachia,” alisema na kuongeza:
“Tumeahidi kutoa Sh10 milioni kwa mtu yeyote, atakayetoa taarifa za mauaji ya Padri Mushi, hii itakuwa kama zawadi tu.”
Habari zilizopatikana zinaeleza kuwa maofisa wa FBI wamekutana
na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Said Mwema kuzungumzia suala hilo la
mauaji ya Padri Mushi.
Tukio hili la kuuawa kwa Padri Mushi linahusishwa
na matukio kadhaa ya vurugu zilizoambatana na uchomaji moto makanisa na
mali mbalimbali hivi karibuni.
Moja ya matukio hayo ni lile la Jumatano ya
Desemba 25 mwaka jana ambapo Padri wa Kanisa Katoliki lililopo Mpendae
visiwani Zanzibar, Ambrose Mkenda, alijeruhiwa kwa risasi na watu
wasiojulikana nje ya nyumba yake, saa 12 jioni wakati akitoka kanisani.
Padri huyo alipatiwa matibabu katika Hospitali Kuu
ya Mnazi Mmoja na baadaye alihamishiwa katika Hospitali ya Taifa
Muhimbili kwa matibabu zaidi.
Wakati huo huo, Sheikh Mussa Ali Mussa ambaye alikuwa kiongozi wa Misikiti ya Kitope na Mwakaje ameuawa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Unguja, Ahmada
Khamis alisema kuwa kiongozi huyo, aliuawa kutokana na kipigo
alichokipata kutoka kwa wezi waliovamia shamba lake.
Kuuawa kwa Sheikh huyo kumezua hofu kwa wakazi wa
Zanzibar wakidhani ni kitendo cha kulipiza kisasi, lakini Polisi
imetuliza hali hiyo kwa kusema kwamba aliuawa na wezi waliokuwa wakiiba
shambani kwake.
Alisema kwamba baada ya kuwafuma wezi hao wakiiba
shambani kwake walimshambulia kwa mapanga na kupoteza uhai wake na
kwamba hadi sasa hakuna mtu aliyekamatwa kuhusiana na tukio hilo.
Habari imeandikwa kwenye mwananchi.co.tz