MWENYEKITI wa CCM, Rais Jakaya Kikwete ameamua kuwatosa vinara
wanaotajwa kutaka kuwania urais kupitia chama hicho kutoingia kwenye
Kamati Kuu (CC).
Dalili za kuwatosa vinara wanaotajwa kuwania urais
2015, ni kutokana na hatua yake ya juzi kuamua kutowapendekeza kuwa
miongoni mwa majina ambayo yangepigiwa kura ili kuweza kuingia katika
CC.
Ndiyo maana baada ya kumalizika Uchaguzi wa
wajumbe wa NEC, Kikwete alisita kuunda CC kwa maelezo kwamba
waliochaguliwa walikuwa wageni na alikuwa hawafamu vizuri. Hatua hii ya
Kikwete ilitafsiriwa kama mkakati wa kuzima nguvu ya mojawapo ya kambi.
Hata
hivyo, kuna mtazamo tofauti kwamba hatua ya Kikwete kutopendekeza
majina makubwa na yenye nguvu ndani ya CCM kuwania ujumbe wa Kamati Kuu
inaweza ikawa ni njia ya kuwafanya wajumbe wa CC kuwa na kazi moja tu
ambayo ni kuchuja majina ya wagombea badala ya wao pia kuwa washiriki.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu Dar es Salaam, Profesa
Gaudence Mpangala alisema kutopendekezwa kwa Lowassa, Membe na Sitta
kulitarajiwa kwa kuwa viongozi wengi wa chama hicho walikuwa hawapendi
jinsi baadhi ya wanachama wa CCM wanavyoonyesha wazi dhamira yao ya
kuutaka urais.
“Inawezekana uamuzi wa CC ukawa na malengo mapana likiwamo hili,
inawezekana chama kiliona kikiyapitisha majina hayo kitaleta mtafaruku
na maneno ya hapa na pale,” alisema Profesa Mpangala.
Mpangala alisema Rais kama Mwenyekiti wa CCM
lazima awe na mipango yake ya kuhakikisha kuwa anatengeneza mtu wa
kuchukua nafasi yake na ambaye wanaelewana.
Naye Mhadhiri mwingine wa
chuo hicho, Bashiru Ally alisema atakayependekezwa kugombea urais ndani
ya CCM, siyo lazima awe mjumbe wa Kamati Kuu au Halmashauri Kuu.
“Ujumbe
tu hautoshi, mtu anaweza asiwe mjumbe wa NEC wala Kamati Kuu, lakini
akawa na ushawishi mkubwa ndani ya vyombo hivyo pamoja na Mkutano Mkuu
wa chama hicho,” alisema Bashiru.
“Wapo wagombea urais mwaka 2005 walienguliwa
licha ya kuwa na majina makubwa, nadhani sifa ya mgombea ndiyo kitu cha
kwanza” alisema Bashiru akitolea mfano wa John Malecela, ambaye alikuwa
Makamu Mwenyekiti wa CCM wakati huo.
Kwa upande wake, mwanasiasa
kijana David Kafulila anaona uamuzi wa Kikwete kutowapendekeza
wanaotajwa kuwania urais ndani ya chama hicho kama mkakati wa kufanya
wajumbe wa CC wawe na kazi moja tu ambayo ni kuchuja wagombea.
“Nadhani Kikwete anaweza akawa na mkakati wa
kufanya wajumbe wa CC wasiwe wachezaji wakati wa kuwania kupeperusha
bendera ya CCM 2015, lakini inaweza ikawa ni mkakati wa kuwapunguzia
nguvu za kutimiza malengo yao,” alisema Kafulila ambaye ni mbunge wa
Kigoma Kusini kwa tiketi ya NCCR-Mageuzi.
Waliochaguliwa kuingia kwenye Kamati Kuu
kutokea Tanzania Bara ni pamoja na Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel
Nchimbi, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo Mijini, Profesa Anna
Tibaijuka na Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais, Steven Wassira.
Wengine
ni Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Bunge), William
Lukuvi, Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Dodoma, Alhaji Adam Kimbisa, Meya
wa Manispaa ya Ilala, Jerry Silaa na Mbunge wa Viti Maalumu, Pindi
Chana.
Kutoka Tanzania Visiwani mbali na Dk Salim,
wengine ni Waziri wa Ulinzi, Shamsi Vuai Nahodha, Waziri wa Mawasiliano,
Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa na Waziri wa Afya na
Ustawi wa Jamii, Dk Hussein Mwinyi.
Pia wamo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa
Rais (Muungano), Samia Suluhu Hassan, Naibu Waziri wa zamani wa
Mawasiliano na Uchukuzi, Dk Maua Abeid Daftari pamoja na Khadija Aboud
Wajumbe wa NEC mtegoni
Rais
Kikwete pia aliwataka wajumbe wa CC na wale wa NEC waheshimu kazi za
wabunge kwenye majimbo yao ili wawape nafasi ya kutekeleza
walichokiahidi.
Akitambulisha wajumbe wapya wa CC, alidai kitendo cha
baadhi ya wajumbe hao kupita katika majimbo na kuanza kufanya kazi za
kuwakosoa wabunge hakifai kuvumiliwa na mara nyingi kinakuwa ni chanzo
cha migogoro na kuwafanya baadhi ya watu kushindwa kutekeleza Ilani ya
CCM.
“Si kwamba msiende hapana, nendeni
mkazungumzie utekelezaji wa Ilani, lakini habari za kuwavuruga wabunge
iwe ni marufuku hadi uchaguzi utakapifika,” aliongeza Kikwete na kumtaka
Makamu Mwenyek iti wa CCM kwa upande wa Tanzania Bara, Phillip Mangula
kuwachukulia hatua kali wahusika.
Kiongozi Bavicha avaa gwanda la kijani
Aliyekuwa
Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chama Cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema) Juliana Shonza jana alimtumia salamu mbunge wa
Ubungo, John Mnyika kuwa asahau ndoto za kulipata jimbo hilo tena.
Mbali
na hilo, aliwataka Watanzania kumpelekea ujumbe kwa wabunge wa Chadema
wa Mkoa wa Mbeya kuwa wakae mkao wa kula kwani hayuko tayari kuona mkoa
aliozaliwa yeye ukiongozwa na Chadema.
Shonza alitoa kauli hiyo jana katika Viwanja
vya CCM Mjini hapa ikiwa ni muda mfupi tangu akabidhi kadi ya Chadema
kwa Kikwete na kujiunga rasmi na CCM.
Mbali na Shonza mwingine
aliyejiunga jana alikuwa ni Mtera Mwampamba ambaye mwaka 2010 alikuwa ni
mgombea ubunge wa Jimbo la Mbozi Mashariki.
Jimbo hilo kwa sasa linaongozwa na Mwenyekiti CCM Mkoa wa Mbeya, Godfrey Zambi.
Huku
akishangilia na umati mkubwa wakazi wa Mji wa Dodoma waliofurika katika
viwanja hivyo, Shonza alianza kwa kumwomba radhi Rais Kikwete kuwa
alikuwa akitumika vibaya kwa kumtukana majukwaani, lakini akasema
anajutia kosa lake na kwamba kwa sasa yuko tayari kumsaidia Rais.
“Nimekosa
Rais, naomba unisamehe mimi na vijana wenzangu, lakini nikiwa na muda
mzuri nitawaeleza Watanzania yaliyoko Chadema na kamwe sijutii uamuzi
huo wa kujiunga na CCM,” alisema
Nape adai wengine wanafuata
Kwa upande
wake, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, alisema kuwa
kuwapokea vijana hao ni mwanzo, lakini Watanzania wategemee kupokea watu
wengi zaidi.
Nape alisema hivi sasa wameanza na kikosi kipya cha
ushindi ambacho walitangaza kuwa ni kikosi cha ushindi mwaka 2015 na
akasema walioko nyuma ya Shonza na Mwampamba ni wengi zaidi.
“Nawakaribisha wananchi siku ya Jumamosi ijayo jijini Dar es
Salaam, lazima tutatikisa kwa kishindo na kuwapokea vijana wengi,
tumeamua na sasa kazi ni moja lazima waishe huko,” alijinasibu Nape.
Chadema wanena
Akizungumzia
kitendo hicho, Mwenyekiti wa Bavicha, John Heche alisema usalama wa
Chadema uko makini zaidi ya Usalama wa Taifa, kwamba haiwezekani wanaCCM
kufanya shughuli za chama hicho akiwa Chadema.
“Huku alikoenda ndio kunamfaa, Chadema na hasa
Bavicha tulijua kuwa (Shonza) alikuwa CCM tangu siku nyingi na
alichokifanya sasa ni kuthibitisha tu,” alisema Heche ambaye aliingia
katika mgogoro wa muda mrefu na Shonza kabla ya kutimuliwa.
Kwa upande wake, Mnyika alisita kuitolea ufafanuzi kauli ya Shonza kwamba anataka kuwania ubunge katika jimbo hilo.
“Ninachoweza kusema ni kwamba (Shonza)
anachotakiwa kufanya ni kupigania apitishwe na chama chake katika kura
za maoni ili awanie ubunge” alisema Mnyika.
Mauaji ya Geita
Naye Rais Kikwete alilaani
mauaji yaliyotokea Geita na kusababisha kifo cha mchungaji wa Kanisa la
Assemblies Of God, Mathayo Kachila (45) na wengine 15 kujeruhiwa katika
machafuko hayo.
Alisema tangu historia ya Tanzania ambayo ni
zaidi ya miaka 50 hapajawahi kutokea mapigano ya udini, lakini sasa
yameonekana kwa mara ya kwanza jambo linalohitaji kila mmoja kulilaani.
Habari kutoka Mwananchi.co