Gari hilo la kubebea wagonjwa liliharibika mitambo yake likiwa njiani ambapo lilikaa dakika 40
Afrika Kusini. Rais wa zamani wa
Afrika Kusini Nelson Mandela maarufu kama Madiba imedaiwa alipata wakati
mgumu wakati akielekea hospitalini baada ya gari la wagonjwa lililokuwa
likimsafirisha wiki mbili zilizopita, kuharibika mitambo likiwa njiani
kwenda hospitalini.
Taarifa za kuharibika kwa gari hilo zilitolewa
juzi na msemaji wa rais wa Afrika Kusini Mac Maharaj, ambaye
alidhibitisha kuwa gari hilo lilipata matatizo na ililazimika Rais
huyo wa zamani kuhamishiwa katika gari nyingine.
Hata hivyo Maharaj, alisema tukio hilo halikuwa na
tishio lolote kwa afya ya mzee Mandela, kwa sababu aliongozana na
madaktari wa kutosha.
Dakika 40
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Marekani CBS
lilisema kuwa vyanzo kadhaa vilidai kuwa Mandela alilazimika kukaa eneo
hilo ambapo gari hilo la wagonjwa liliharibika kwa muda wa dakika 40.
Shirika hilo la CBS lilisema kuwa wakati Mandela alipokuwa
akihamishwa katika gari nyingine viwango vya joto vilikuwa chini sana.
Mandela alilazwa hospitalini huku hali yake ikiwa
mbaya kutokana na maambukizi ya mapafu ya mara kwa mara na tangu wakati
huo alikuwa katika chumba cha wagonjwa mahututi.
Hii ni mara ya tatu kwa Mandela kulazwa hospitalini mwaka huu.
Mandela, aliye na umri wa miaka 94, alilazwa
hospitalini mnamo Juni 8, baada ya kupata matatizo ya kupumua, ugonjwa
ambao umekuwa ukimsumbua mara kwa mara.
Akiongea na Shirika la Habari la Enca, Mac Maharaj
alisema kuwa ‘hakuna tatizo lililotokea’ kwani walikuwa makini, wakati
wa tukio hilo.
Alipotakiwa kutoa maelezo kwamba ilikuwaje gari la
kubebea wagonjwa ilitumike ikiwa na hitilafu za kimitambo alisema
“Hili ni tukio la kawaida. Hakuna anayeweza kutarajia kuwa gari
lililokuwa likienda vizuri lingeweza kukumbwa na hitilafu za kimitambo.”
Ini na figo
Taarifa za ndani zilisema kwamba ini na figo za
rais huyo wa zamani zilikuwa zikifanya kazi kwa asilimia 50. Kiongozi
huyo vile vile alitarajiwa kufanyiwa upasuaji maalumu kuziba kidonda
kilichokuwa kikivunja damu.
Kwa mujibu wa mjukuu wa Madiba, Ndaba Mandela
alisema babu yake alikuwa akiendelea vyema na alikuwa akitarajiwa kuwa
atatoka hospitalini hivi karibuni.
“Ni Mungu pekee anayeweza kumchukua…sisi kama familia tutazidi kushukuru na kusherekea maisha yake,”alisema Ndaba Mandela.
Wakati huohuo mmoja wa wanaharakati wa kupinga
ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini Dk. Ramphele amezindua chama kipya
cha kisiasa kutoa changamoto kwa chama tawala cha ANC kwenye uchaguzi
mkuu wa nchi hiyo hapo mwakani.
Dk. Ramphele aliwaambia wafuasi wake
waliokusanyika wakati wa uzinduzi wa chama hicho mjini Pretoria kuwa ANC
haitakiwi kuaminiwa kuinua uchumi wa nchi hiyo.
Chama chake kijulikanacho kama Agang chenye maana
ya kujenga kimejipanga kupigana na rushwa na kuimarisha sekta ya elimu
kama malengo yao makuu.
Dk Ramphele ni mkurugenzi wa zamani wa Benki ya Dunia na ni mke wa zamani wa mpigania uhuru wa Afrika Kusini hayati Steven Biko
Habari kutoka gazeti la mwananchi