Thursday, June 27, 2013

Membe: Msije Dar wakati wa ziara ya Obama


Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe amewashauri watu walioko mikoani kusitisha safari za kuja Dar es Salaam wakati wa ziara ya Rais wa Marekani, Barrack Obama kutokana na wingi wa wageni katika jiji hilo.
Ugeni huo pamoja na ule wa viongozi kumi na moja kutoka nchi mbalimbali duniani watakaohudhuria mkutano wa kimataifa wa Smart Partnership utakaofunguliwa kesho na Rais Jakaya Kikwete kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere, umesababisha kuimarishwa kwa ulinzi katika maeneo mbalimbali hasa katika hoteli za kitalii ambazo zimeanza utaratibu wa upekuzi kwa wageni wake.
Akizungumza na katika mahojiano na Redio ya Clouds jana, Membe alisema jiji limefurika kwa wingi wa wageni.
“Hoteli na nyumba za wageni zimefurika wageni na magari mengi yamekodiwa. Kwa ujumla, huduma za kijamii zitakuwa shida,” alisema.
Rais Obama na mkewe Michelle watawasili nchini Jumatatu na tayari wapambe na maofisa usalama kutokana Marekani wameanza kuwasili. Mbali ya ujio huo, wake wa marais kutoka nchi 14 za Afrika watakaokutana na Laura Bush, mke wa Rais wa zamani wa Marekani, George Bush. Pia Michelle atahudhuria mkutano huo utakaofanyika Jumanne na Jumatano ijayo.
“Jiji la Dar es Salaam litakuwa na mambo mengi kwa hiyo wale wenye kuja kutaka kustarehe wafute safari zao,” alisema na kuongeza: “Kama kuna watu ambao hawapo Dar es Salaam na hawana sababu za kuja mjini waache tu mpaka wageni watakapoondoka kwa sababu jiji la litakuwa limejaa na baadhi ya barabara zitachukuliwa zitumike na wageni hao.”
Alisema katika kipindi cha siku tano zijazo, baadhi ya barabara za Jiji la Dar es Salaam zitakuwa na shughuli nyingi na nyingine zitalazimika kufungwa. Barabara itakayofungwa ni pamoja na ile ya Mwai Kibaki na ile ya Bagamoyo itakuwa na shughuli nyingi pia wakati Michelle atakapokwenda Jumba la Makumbusho, Jumanne ijayo.
Wasafiri wa mikoani
Wasafiri wa mikoani wataathirika zaidi Jumanne ijayo wakati Rais Obama atakapokwenda kutembelea mitambo ya kufua umeme ya Kampuni ya Symbion Ubungo.
Kituo hicho kipo Barabara ya Morogoro, ambayo ndiyo inayotumiwa na magari yanayoingia na kutoka mikoani.
Rais Obama atakwenda katika kituo hicho yapata saa 4.00 asubuhi na kwa kiasi kikubwa itaathiri magari ya usafirishaji wa mizigo na abiria yatakayokuwa yanatoka na kuingia Dar es Salaam kabla na wakati huo.


Wengine watakaoathirika ni wakazi wa Kimara, Mbezi, Kibamba hadi Kiluvya. Athari nyingine ya usafiri itakuwa katikati ya jiji ambako Obama na msafara watakuwa na shughuli nyingi na hasa ile ya ufunguzi wa barabara karibu na Ikulu na kukutana na wafanyabiashara kwenye Hoteli ya Hyatt Regency, Jumatatu ijayo.
Watumiaji wengine wa barabara watakaopata shida ni wale wa Barabara ya Bagamoyo hasa pale Rais Obama na mkewe watakapokwenda kuweka mashada ya maua kwenye ubalozi wa zamani wa Marekani uliopuliwa na mabomu mwaka 1998.
Ulinzi hoteli za kitalii
Mashushushu wa ndani na nje ya nchi wamezingira kwenye hoteli kubwa za Dar es Salaam na walionekana katika baadhi ya hoteli hizo, wakiwatumia mbwa maalumu kufanya ukaguzi wa chumba hadi chumba.
Tofauti na utaratibu uliozoeleka, baadhi ya hoteli zenye hadhi ya nyota tano zimeanza kutumia mitambo maalumu ya kompyuta kuwafanyia ukaguzi wageni wote wanaoingia.
Wamchongea JK
Mtandao wa Kutetea Waandishi wa Habari Duniani (CPJ), umemwandikia barua Rais Obama ukimtaka kujadiliana kwa kina na mwenyeji wake Rais Kikwete wakati wa ziara yake nchini kuhusiana na vitendo vya kuuawa na kuteswa kwa waandishi wa habari wa Tanzania.
Katika barua hiyo iliyosainiwa na Mtendaji Mkuu wa CPJ, Joel Simon na nakala yake kusambazwa kwa viongozi mbalimbali akiwemo Rais Kikwete mwenyewe, mtandao huo ulitolea mfano wa kuuawa kwa Mwandishi wa Channel 10, Daudi Mwangozi na Issa Ngumba wa Redio Kwizera. Pia kupigwa na kuteswa kwa Mhariri Mtendaji wa Habari Corporation, Absalom Kibanda.


Akizungumzia mkutano wa Smart Partnership utakaoanza kesho, Membe alisema utajadili jinsi ya kutumia sayansi na teknolojia kukuza uchumi.
Viongozi watakaohudhuria mkutano huo ni Waziri Mkuu wa Malayasia, Najib Razak, Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, Uhuru Kenyetta (Kenya), Boni Yayi (Benin), Ali Omar Bongo (Gabon), Ikililou Dhoinine (Comoro), Faure Gnassingbe (Togo), Ernest Koroma (Sierra Leone), Blaise Compaore (Burkina Fasso), Mahinda Rajapaska (Sri Lanka) na Mfalme wa Swaziland, Mswati II, ambaye aliwasili jana.

Habari kutoka gazeti la Mananchi
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...