na Betty Kangonga
KUTEKWA,
kupigwa na kuteswa kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Chama cha Madaktari
nchini, Dk. Steven Ulimboka na hatimaye kufungiwa kwa Gazeti la
MwanaHalisi kwa muda usiojulikana, kumeleta kizaazaa katika kampuni ya
simu za mkononi ya Tigo, Tanzania Daima Jumatano limebaini.
Habari
kutoka ndani ya kampuni hiyo ya simu yenye mtandao mpana nchini,
zinasema kuwa zaidi ya wafanyakazi 30 wamefukuzwa kazi na wengine wako
kwenye uchunguzi wakituhumiwa kuvujisha mawasilino ya siri ya simu za
wateja kwa Gazeti la MwanaHalisi.
Kwa
mujibu wa habari hizo, taarifa za mawasiliano za simu zinazodaiwa
kuvujishwa na wafanyakazi hao, zilikuwa kati ya Dk. Ulimboka, Afisa
Usalama wa Ikulu na watu aliowasiliana nao kabla ya kutekwa.
Rais
Jakaya Kikwete amepata kuliambia taifa mara mbili kwa njia ya
televisheni, mwishoni mwa Juni na alipozungumza na wahariri wa vyombo
vya habari wiki iliyopita, kwamba serikali yake haihusiki kuteka, kutesa
na kumtupa daktari huyo porini.
Naye
Waziri Mkuu Mizengo Pinda amepata kuliambia Bunge kuwa, serikali yake
haihusiki na utekaji, utesaji na kuhoji, “...serikali imteke ili iweje?”
Hivi
karibuni serikali ililifungia Gazeti la MwanaHalisi baada ya kuandika
habari iliyomtaja ofisa mmoja wa Idara ya Usalama wa Taifa Ikulu (TISS),
kuwa ndiye aliyetekeleza mpango wa kumteka, kumpiga na kumtesa hadi
kumjeruhi Dk. Ulimboka, ambaye kwa sasa anaendelea na matibabu kwenye
hospitali moja nchini Afrika Kusini.
Kwa
mujibu wa habari hiyo ambayo serikali inadai kuwa ni ya uchochezi,
MwanaHalisi ilianika namba ya simu ya ofisa huyo pamoja na watu wengine
wanaodaiwa kuhusika katika tukio hilo linaloendelea kuchunguzwa na
kamati maalumu iliyoundwa na Ofisi ya Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai
(DCI).
Vyanzo
vya habari kutoka kwa baadhi ya wafanyakazi waliokumbwa na sekeseke
hilo, zinasema kuwa waliofukuzwa wengi ni wafanyakazi wa kitengo cha IT
ambao wanadaiwa kuhusika kutoa taarifa za siri ya mawasilino kati ya Dk.
Ulimboka na watu wanaoaminika kuwa ni wabaya wake.
Mmoja
wa wafanyakazi kutoka Kampuni ya Tigo, aliliambia gazeti hili kuwa
mbali na kutuhumiwa kutoa siri kwa Gazeti la MwanaHalisi, wafanyakazi
wengine wametimuliwa kwa madai ya kufanya udanganyifu kwenye huduma za
Tigo Pesa na kujipatia fedha.
“Kweli
watu wengi wamefukuzwa wakituhumiwa kutoa siri kwa Gazeti la
MwanaHalisi, lakini wengine walikuwa wakishirikiana na mawakala wa Tigo
Pesa kuiibia kampuni.
“Kwa
mfano mfanyakazi alikuwa anakubaliana na wakala kumwingizia kiasi kama
cha sh milioni moja, lakini anaweza kuingiza hadi sh milioni 1.5 na kati
ya hizo sh 500,000 ni mali yake,” alisema mfanyakazi huyo.
Akizungumzia
na Tanzania Daima Jumatano, Mhariri Mkuu wa Gazeti la MwanaHalisi,
Jabir Idrissa alishangazwa na taarifa za Tigo kuwafukuza wafanyakazi
wake kwa sababu ya habari iliyochapishwa na gazeti lake.
“Chanzo
chetu cha habari hakikutoka kwa wafanyakazi wa Tigo. Kama wamefukuzwa
kwa sababu ya MwanaHalisi, wamewaonea bure. Kama Tigo ndio waliotupa
taarifa na zile za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), zilitoka wapi?”
alihoji Jabir na kusisitiza wafanyakazi hao wameonewa bure.
Ofisa
Uhusiano wa Tigo, Edward Shila, alipohojiwa kuzungumzia tukio hilo,
hakukubali wala kukataa madai hayo na kumtaka mwandishi kumtumia maswali
kupitia e-mail yake ili aweze kuyatolea majibu kiofisi.
“Kama
una maswali naomba uniandikie kupitia e-mail yangu ambayo nakutumia
sasa hivi…maana siko tayari kutoa kauli yoyote isiyokuwa ya kiofisi,”
alisema.
Naye
Omary Matulla ambaye amejitambulisha kuwa ni ofisa wa kitengo cha
kumbukumbu katika kampuni hiyo, alikanusha kuwapo kwa taarifa za
kufukuzwa wafanyakazi wa kampuni hiyo.
Alisema
kuwa kila mfanyakazi ana mipaka ya kufanya kazi katika kampuni hiyo, na
pia ni wajibu wa kila mtumishi kutunza siri kubwa.
“MwanaHalisi
ana mbinu zake za kupata habari wala haiwezekani kupata habari kupitia
kampuni yetu na hata hivyo jambo hilo si rahisi hata kidogo kutokea,”
alikanusha Omary.
Dk.
Ulimboka alitekwa usiku wa Juni 26, kusukumizwa kwenye gari, kupigwa,
kufungwa mikono na miguu, kunyofolewa kucha na kutolewa meno na hatimaye
kutupwa katika msitu wa Mabwepande nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Tangu
kutokea kwa tukio la kutekwa kwa Dk. Ulimboka, Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (CHADEMA) na wanaharakati wa kutetea haki za binadamu,
wamekuwa wakiinyoshea kidole serikali kwamba ndiyo iliyohusika.
Kamanda
wa Kanda Maalumu ya Polisi mkoani Dar es Salaam, Suleiman Kova, hivi
karibuni alitangaza kumfikisha mahakamani mtu mmoja aliyedai kukiri
kuhusika na utekaji wa Dk. Ulimboka.
Kova
aliwaambia waandishi wa habari kuwa, polisi wamekamata mtu aitwaye
Joshua Malundi kutoka Kenya ambaye amekiri kumteka na kumtesa Dk.
Ulimboka.
Alidai kuwa mtuhumiwa alikwenda kutubu katika Kanisa la Ufufuo na Uzima, Kawe, Dar es Salaam.
Lakini
hata hivyo, mchungaji wa kanisa hilo, Josephat Gwajima alikana kauli ya
Kova juu ya mtuhumiwa huyo, akisema hajakwenda kutubu kwao.
Source: Tanzania Daima