na Tamali Vullu, Dodoma
SERIKALI imesema katika mwaka huu wa fedha, itatengeneza ajira 800,000 katika fani mbalimbali nchini.
Kauli
hiyo ya serikali ilitolewa bungeni jana na Waziri wa Kazi na Ajira,
Gaudensia Kabaka, alipokuwa akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi
kwa wizara yake kwa mwaka 2012/2013.
Alisema
fursa za ajira hizo mpya zitapatikana kupitia miradi ya maendeleo chini
ya mpango wa taifa wa miaka mitano unaotekelezwa na wizara na taasisi
mbalimbali ((FYDP I).
“Takwimu
hizi ni mbali na ajira za watumishi 56,678 watakaoajiriwa na serikali
kama ilivyobainishwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya
Utumishi wa Umma, ” alisema.
Waziri Kabaka alisema ajira hizo zitapatikana katika sekta za kilimo, ujenzi, mawasiliano na viwanda.
“Ajira
zitakazozalishwa katika Kilimo ni 169,189, ujenzi wa miundombinu ya
barabara 646,615, mawasiliano 27,600 na katika sekta ya viwanda na
biashara zitazalishwa ajira 5,000,” alisema.
Alibainisha kuwa katika mpango huo wa kuongeza ajira, halmashauri za mikoa ya Dar es Salaam na Pwani zitazalisha ajira 6,885.
Alieleza kuwa katika mwaka wa fedha ulioisha, jumla ya ajira 250,678 zilipatikana kutokana na miradi ya maendeleo.
Alisema
ajira zilizopatikana katika miradi mbalimbali ikiwemo Tasaf (34,516),
ujenzi wa barabara (42,107) na ujenzi wa majengo ya serikali (17,685).
Miradi
mingine kituo cha taifa cha uwekezaji (TIC) ajira 82,834, mamlaka ya
ukanda wa kiuchumi (EPZA) 15,100 na serikali ilitengeneza ajira 38,289.
Source: Tanzania Daima