Dar es Salaam. Ikulu ya Marekani na Idara ya 
Habari (Maelezo), wametangaza ratiba ya Rais Barrack Obama atakapozuru 
Tanzania huku ikionyesha kuwa atakaa siku mbili tu, kuanzia Julai Mosi 
na kuondoka kesho yake.
Tanzania itakuwa nchi ya mwisho ya Afrika 
kutembelewa na Obama baada ya Senegal na Afrika Kusini. Mara 
atakapowasili na ndege yake kubwa ya Air Force One, Rais Obama atazindua
 barabara mpya katika upande wa Mashariki wa geti la kuingia Ikulu.
Rais Obama, ambaye atafuatana mkewe Michelle pia 
siku hiyohiyo atazungumza kwa nyakati tofauti na  wafanyabiashara kutoka
 nchi za Afrika na Marekani kwenye Hoteli ya Hyatt Regency, Dar es 
Salaam.
  
“Pia amepanga kuzungumza na maofisa wa Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania,” ilisema taarifa ya Maelezo.
Baada ya shughuli hiyo, Rais Obama atahudhuria 
dhifa ya taifa atakayoandaliwa Ikulu na mwenyeji wake, Rais Jakaya 
Kikwete. Siku itakayofuata ataweka shada la maua kwenye sehemu ulipokuwa
 Ubalozi wa Marekani ikiwa ni kumbukumbu ya watu waliofariki katika 
shambulizi la bomu mwaka 1998. Pia atatembelea mitambo ya kufua umeme ya
 Kampuni ya Symbion na atatoa hotuba akizungumzia mikakati ya Marekani 
ya kulisaidia Bara la Afrika kuzalisha nishati ya umeme.
“Tanzania ni mshirika muhimu wa Marekani,” alisema
 Ofisa wa Ikulu ya Marekani, Ben Rhodes wakati alipozungumza na 
waandishi wa habari mwishoni mwa wiki katika Ikulu ya Marekani kuhusu 
ratiba ya ziara ya Obama barani Afrika.
Pia mke wa Obama atakuwa na ratiba yake. Julai 
Mosi, atapata staftahi na mwenyeji wake, Salma Kikwete katika ofisi za 
Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (Wama), Dar es Salaam.
Pia atatembelea sehemu ubalozi wa zamani wa 
Marekani na baadaye atashuhudia onyesho la utamaduni la Kikundi cha Baba
 wa Watoto, ambacho kinajumuisha watoto wa mitaani wenye umri kuanzia 
miaka mitano hadi 18 kwenye Makumbusho ya Taifa. Julai 2, atahudhuria 
mkutano na wake wa marais wa nchi za Afrika ambao pia utahudhuriwa na 
mke wa Rais wa zamani wa Marekani, George Bush, Laura.
Habari kutoka gazeti la Mwananchi
Habari kutoka gazeti la Mwananchi


 
 









 
 
 
 
