Gari hilo la kubebea wagonjwa liliharibika mitambo yake likiwa njiani ambapo lilikaa dakika 40
Afrika Kusini. Rais wa zamani wa 
Afrika Kusini Nelson Mandela maarufu kama Madiba imedaiwa alipata wakati
 mgumu wakati akielekea hospitalini baada ya gari la wagonjwa lililokuwa
 likimsafirisha wiki mbili zilizopita, kuharibika mitambo likiwa njiani 
kwenda hospitalini.
Taarifa za kuharibika kwa gari hilo zilitolewa 
juzi na msemaji wa rais wa Afrika Kusini Mac Maharaj, ambaye 
alidhibitisha kuwa gari hilo lilipata  matatizo na ililazimika  Rais 
huyo wa zamani kuhamishiwa katika gari nyingine.
Hata hivyo Maharaj, alisema tukio hilo halikuwa na
 tishio lolote kwa afya ya mzee  Mandela, kwa sababu aliongozana  na 
madaktari wa kutosha.
Dakika 40
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Marekani CBS  
lilisema kuwa vyanzo kadhaa vilidai kuwa Mandela alilazimika kukaa eneo 
hilo ambapo gari  hilo la wagonjwa liliharibika kwa muda wa dakika 40.
 
Shirika hilo la CBS lilisema kuwa wakati Mandela alipokuwa 
akihamishwa katika  gari nyingine viwango vya joto vilikuwa chini sana.
Mandela alilazwa hospitalini huku hali yake ikiwa 
mbaya kutokana na maambukizi ya mapafu ya mara kwa mara na tangu wakati 
huo alikuwa katika chumba cha wagonjwa mahututi.
Hii ni mara ya tatu kwa Mandela kulazwa hospitalini mwaka huu.
Mandela, aliye na umri wa miaka 94, alilazwa 
hospitalini mnamo Juni 8, baada ya kupata matatizo ya kupumua, ugonjwa 
ambao umekuwa ukimsumbua mara kwa mara.
Akiongea na Shirika la Habari la Enca, Mac Maharaj
 alisema kuwa ‘hakuna tatizo lililotokea’ kwani walikuwa makini, wakati 
wa tukio hilo.
Alipotakiwa kutoa maelezo kwamba ilikuwaje gari la
 kubebea wagonjwa  ilitumike ikiwa  na hitilafu za kimitambo  alisema  
“Hili ni tukio la kawaida. Hakuna anayeweza kutarajia kuwa gari 
lililokuwa likienda vizuri lingeweza kukumbwa na hitilafu za kimitambo.”
Ini na figo
Taarifa za ndani zilisema kwamba  ini na figo za 
rais huyo wa zamani zilikuwa zikifanya kazi kwa asilimia 50. Kiongozi 
huyo vile vile alitarajiwa kufanyiwa upasuaji maalumu  kuziba kidonda 
kilichokuwa kikivunja damu.
Kwa mujibu wa mjukuu wa  Madiba, Ndaba Mandela 
alisema babu yake  alikuwa akiendelea vyema na alikuwa akitarajiwa kuwa 
atatoka hospitalini hivi karibuni.
 “Ni Mungu pekee anayeweza kumchukua…sisi kama familia tutazidi kushukuru na kusherekea maisha yake,”alisema  Ndaba Mandela.
Wakati huohuo mmoja wa wanaharakati wa kupinga 
ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini Dk. Ramphele amezindua chama kipya
 cha kisiasa kutoa changamoto kwa chama tawala cha ANC kwenye uchaguzi 
mkuu wa nchi hiyo hapo mwakani.
Dk. Ramphele aliwaambia wafuasi wake 
waliokusanyika wakati wa uzinduzi wa chama hicho mjini Pretoria kuwa ANC
 haitakiwi kuaminiwa kuinua uchumi wa nchi hiyo.
Chama chake kijulikanacho kama Agang chenye maana 
ya kujenga kimejipanga kupigana na rushwa na kuimarisha sekta ya elimu 
kama malengo  yao makuu.
Dk Ramphele ni mkurugenzi wa zamani wa Benki ya Dunia na ni mke wa zamani wa mpigania uhuru wa Afrika Kusini hayati Steven Biko
Habari kutoka gazeti la mwananchi 


 
 









 
 
 
 
