Friday, March 1, 2013

MSEMO WA ‘KUFELI MTIHANI SIYO KUFELI MAISHA’ UNAVYOWAHARIBU VIJANA!-2


NINA kila sababu ya kumshukuru Mungu ambaye amenibariki kuwa mmoja kati ya wale waliobahatika kuiona siku ya leo wakiwa bukheri wa afya.
Ni matumaini yangu kuwa, nawe umzima na uko tayari kusoma sehemu ya pili ya makala haya ambayo niliianza wiki iliyopita.
Lengo hasa la makala haya ni kuonyesha umuhimu wa elimu katika maisha ya leo. Usipokuwa umeelimika maisha yako hayawezi kwenda sawa, utakwenda lakini utafika mahali utakwama.
Ndiyo maana nikaona niwakumbushe wale wanaoona kuwa elimu haina faida wasijidanganye na nisisitize tu kwamba, msemo wa kufeli mtihani siyo kufeli maisha hauna mantiki yoyote.
Tusijipe matumaini kwa njia hiyo kwani ni ukweli usiyofichika kwamba, elimu ni kitu muhimu sana katika ulimwengu wa sasa na waliyoikosa tunashuhudia wanavyohangaika.
Juzijuzi hapa yalitangazwa matokeo ya kidato cha nne. Tumeona wengi walivyofeli. Huu ni msiba mkubwa kwa taifa. Cha ajabu sasa wakati watu makini wakijadili chanzo cha kufeli huko, wapo ambao wala hawajali, wanaamini kufeli kwao hakuna madhara yoyote.
Ndiyo maana wakati mwingine unaweza kukuta mwanafunzi ana uwezo mzuri wa kufaulu kama atasoma kwa bidii na kujiwekea malengo lakini kinyume chake anachukulia kusoma kama fasheni na wala hajali pale anapopata alama mbaya.
Hajali kwa kuwa ameshajiwekea akilini mwake kwamba, hata asipofaulu maisha yake yanaweza kuwa poa tu huku akitolea mfano wale ambao hawakusoma lakini leo wana maisha mazuri.
Wengine utawasikia wakisema: Aah! Mbona fulani alipata ziro lakini mambo yake ni safi? Mbona fulani aliishia darasa la saba lakini sasa ni tajiri?” Jamani hiyo ni bahati ya mtu. Usitarajie kwa sababu mwenzako mambo yake yamemnyookea bila ya ya kwenda shule basi na wewe unaweza kuwa hivyo.
Huko ni kujidanganya. Wengi ambao hawakusoma au walikwenda shule lakini wakazembea na hatimaye kufeli hawana maisha mazuri. Hao ndiyo wamekuwa na maisha ya kushinda vijiweni huku wakipiga mizinga kwa kila mtu anayekatiza mbele yao.
Ni wasomi wachache sana ambao hawana maisha mazuri na ukifuatilia utabaini kuwa, walizembea na kushindwa kutumia elimu zao katika kuyaboresha maisha yao.
Nimalizie kwa kushauri tu kwamba, elimu ina umuhimu mkubwa sana katika maisha hivyo unapopata nafasi ya kusoma, soma kwa bidii na hakikisha unafanya vizuri.
Pia itumie elimu yako vilivyo kuhakikisha unakuwa na maisha mazuri ili kujitofautisha na waliokimbia umande.
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...