Thursday, May 3, 2012

MALI ZA KANUMBA ZAANZA KUUZWA


Na Shakoor Jongo

SIKU ishirini na sita zimekatika tangu nyota wa sinema Tanzania, Steven Charles Kanumba ‘The Great’ afariki dunia, kuna taarifa kwamba mali zake zimeanza kuingia kwenye mauzo.
Kwa mujibu wa chanzo chetu cha habari, mama mzazi wa marehemu Kanumba, Flora Mtegoa anasaka mteja wa kulinunua gari aina ya Toyota Lexus lenye namba za usajili T750 AER lililoachwa na staa huyo mkubwa ndani na nje ya Bongo.
CHANZO CHAMWAGA SIRI
Chanzo hicho kimesema gari hilo limeingia sokoni likisimamiwa na mwanamke mmoja (jina linahifadhiwa) ambaye amekabidhiwa ‘dokumenti’ zote.
“Jamani gari la marehemu Kanumba lile ambalo alikuwa anatambiana na Ray (mwigizaji Vincent Kigosi) linauzwa. Yupo mwanamke mmoja amepewa kazi hiyo na amekabidhiwa makaratasi yote yenye maelezo,” kilisema chanzo.
Kikaendelea: “Mama wa marehemu ndiye aliyeamua hivyo, tayari siku ya Jumanne (juzi) kuna wateja walijitokeza, lakini baada ya makubaliano walitaka kujiridhisha kwa kwenda kwenye ‘yadi’ ambayo Kanumba alipolinunua gari lile, pale Sozmy maeneo ya Kijitonyama, Dar.”
Inadaiwa lengo la wanunuzi hao kwenda yadi ni kutaka kujua kama marehemu Kanumba hakuwa akidaiwa na waliomuuzia gari hilo.
Kuhusu bei, chanzo kilisema kwa mteja anayelitaka anatakiwa kuweka mezani Sh. milioni 45 ili akabidhiwe gari hilo.
Awali, marehemu Kanumba alisema alilinua gari hilo kwa Sh. milioni 78 hivyo kuuzwa kwa bei ya mama ni pungufu ya Sh. milioni 33.
MALI NYINGINE ZIKAE TAYARI
Hata hivyo, kwa mujibu wa habari za ndani, kuuzwa kwa gari hilo ni mwanzo wa maandalizi ya kuendelea kupigwa bei kwa mali nyingine za marehemu ili kuweka sawa maisha ya familia kufuatia kifo cha msanii huyo.

KWA WENZETU WA NJE
Kule majuu nchi za Ulaya na Marekani, utaratibu wa mali za marehemu kama alikuwa supastaa hupigwa mnada hadharani ambapo bei huwa juu kupita ya manunuzi ya awali.
Kama familia ya Kanumba ingeamua kupiga mnada gari hilo kuna uwezekano lingenunuliwa kwa zaidi ya Sh. milioni 100.

KUNA USIRI?
Haijajulikana mara moja sababu za kuuzwa kwa gari hilo ndani ya kipindi cha kuelekea 40 ya marehemu Kanumba aliyefariki dunia Aprili 7, mwaka huu nyumbani kwake, Vatican City Hotel, Sinza, Dar.
Taratibu za jamii ya Kitanzania, mali za marehemu hujulikana hatima yake kwenye 40 ambapo hutafutwa mrithi wake.

Ziko pia habari kwamba baba mzazi wa marehemu Kanumba, Mzee Charles Kusekwa Kanumba anayeishi Shinyanga amepanga kupata mgawo wa mali za marehemu huku akisema anajua kila kitu kilichoachwa na mwanaye.
Mzee huyo alipovutiwa simu na paparazi wetu kuulizwa kama ana habari yoyote kuhusu mali za marehemu kuuzwa alijibu atafuatilia.
“Sina taarifa yoyote ila nitafuatilia ili nione hilo likoje,” alisema.
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...