Thursday, May 3, 2012

A-Z BARAZA JIPYA LA MAWAZIRI

                                                              Rais Jakaya Kikwete.
Na Elvan Stambul

RAIS Jakaya Kikwete amekasirishwa na utendaji mbovu wa baadhi ya mawaziri wa serikali yake hivyo kuamua kulivunja baraza lake la mawaziri.
Habari kutoka chanzo chetu ndani ya Ikulu zinasema Rais Kikwete amehuzunishwa na ubadhirifu uliofanywa na baadhi ya viongozi wa serikali, hali iliyomfanya aseme wazi kwamba hakufurahishwa na watu ambao wanachukua fedha za umma ili kunenepesha matumbo yao.


Habari zaidi zinasema kuwa kutokana na ulaji wa fedha za umma ambao Kikwete alisema ni kama wa mchwa, uliofanywa na baadhi ya viongozi wasiokuwa na huruma na wananchi, kuna uwezekano mkubwa wa watuhumiwa kupandishwa kizimbani.

“Hawa watu watachukuliwa hatua za kisheria ili kulinda heshima ya chama chake (Chama Cha Mapinduzi) na serikali yake. Nakuhakikishia kuwa hili limemkera sana rais na hata kile kitendo cha mawaziri kubishana hadharani,” kilisema chanzo hicho. Hadi wakati tunakwenda mitamboni kulikuwa na tetesi kwamba Rais Kikwete angetangaza baraza lake jipya la mawaziri wakati wowote.

Bunge katika kikao chake kilichopita lilipendekeza kwa serikali kuwa mawaziri wanane watimuliwe na wakatishia kuwa wasipotimuliwa watampigia kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu Mizengo Pinda kutokana na ubadhirifu wa fedha ulioainishwa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali, Ludovic Utouh.
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...