Wednesday, August 10, 2011

Maaskofu 10 jela maisha

  

Maaskofu 10 kati ya 12 Bongo wanaojihusisha na biashara ya madawa ya kulevya hawana namna ya kuchomoka, serikali imewalenga na shabaha zimekubali, hivyo wanachongoja ni adhabu kali inayoweza kufikia kifungo cha maisha jela.

Habari za kiuchunguzi zinasema kuwa, maaskofu wawili wanaweza kupona kwa sababu ushahidi haujajitosheleza lakini 10 hawana ujanja, kwa hiyo wapo kwenye mkondo wa kupokea adhabu ya kifungo cha maisha jela watakapofikishwa mahakamani na kukutwa na hatia.

Katika ‘kusapoti’ uchunguzi wetu, wiki iliyopita, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais,( Sera na Uratibu wa Bunge), William Lukuvi aliwaahidi wabunge kwamba ushahidi utakaoambatana na mkanda wa video utapelekwa bungeni ili waheshimiwa hao wajionee jinsi baadhi ya viongozi wa dini walivyokosa maadili.

Lukuvi alikazia kuwa viongozi hao wa dini, wengi wao wapo chini ya mtandao unaoongozwa na askofu mkubwa kutoka Nigeria ambaye ameshanaswa na hivi sasa anaishi nyuma ya nondo za moja ya magereza yetu.

Mkuu wa Kitengo cha Kudhibiti Madawa ya Kulevya katika Jeshi la Polisi nchini, Godfrey Nzowa aliliambia gazeti hili wikiendi iliyopita kwamba mtu anayekutwa na hatia ya kujihusisha na biashara ya madawa ya kulevya adhabu ya juu kabisa ni kifungo cha maisha jela.

Nzowa alisema: “Tumekuwa wakali sana, tunasimamia kifungo cha maisha jela ili kukomesha biashara hii haramu. Inawezekana hakimu akapima kosa la mshtakiwa na kumhukumu miaka 30 jela lakini ukweli ni kwamba sasa hivi adhabu ya juu ni kifungo cha maisha jela.”

Hata hivyo, kama ilivyokuwa kwa Lukuvi, Nzowa alikataa kutaja majina ya viongozi wa dini wanaotuhumiwa kuwa ‘wazungu wa unga’ lakini alisisitiza kwamba kila kitu kinakwenda kwa hatua na kwamba arobaini yao imefika bila chenga.

“Majina hatutayatoa kwa vyombo vya habari kwa sasa, tupo makini sana. Wakati ukifika mtawaona wahusika na hatutanii, tuna vielelezo vya kutosha kuwatia hatiani,” alisema Kamanda Nzowa.

source--global publisher

0 comments:

Post a Comment

CHANGIA MAWAZO YAKO HAPA

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...