Sunday, January 27, 2013

BARUA YA MDAU WA AMANI KWA MH.BABA RIDHWANI KUHUSIANA NA SAKATA LA MTWARA

Katika pita pita yangu kwenye mtandao wa kijamii wa JAMII FORUM nimekutana na barua hii ya mdau mmoja kwa mh raisi nikaamua nishee na ninyi ndugu zangu kutokana na maneno mazito na ya busara aliyoyaongea mdau huyo,hii hapa isomeni;

Mheshimiwa Rais,

Najua uko bize ofisini kwako ukiendelea kutekeleza majukumu uliyopewa na Watanzania tangu 2010. Au pengine uko nchi fulani ukitembea huku na kule kuaangalia hili na lile ambalo wenzetu hao wameweza kulijenga. Au labda, kwa sababu leo ni wikiendi, uko katika ukumbi mmojawapo wa starehe hapo Magogoni ukipata kinywaji pamoja na wasaidizi wako.

Mheshimiwa Rais, najua unafika Jamii Forums mara kadhaa. Ama, kama wewe binafsi hufiki humu, wasaidizi wako wataisoma barua hii na kukufikishia ujumbe wangu. Ujumbe wangu waweza usitofautiane sana na jumbe nyingi zilizojaa vilio na machozi, ambavyo hata hivyo hukuvijali sana. Hata hivyo ujumbe huu ni wa muhimu kwako hasa kwa sababu unahusu wewe, pamoja na serikali yako kwa ujumla. Waweza kuupuuza kama ulivyozoea, ila tambua kuwa utakapoupuuza ujumbe huu, kuna siku utaukumbuka maana kwa hakika hali ya nchi si shwari.

Mheshimiwa Rais, matatizo yanapozidi, mioyo ya watu huota sugu. Kuna matukio kadhaa ambayo yameshatokea katika nchi yetu. Sitaki kuzungumzia ya nyuma ila nakukumbusha tu kuwa kuna mauaji ya watu watatu kule Arusha, mtu mmoja kule Morogoro, mwandishi wa habari kule Iringa, mtu mwingine kule Arumeru Mashariki, mtu mwingine kule Singida, na maeneo mengine mengi. Nikukumbushe pia mabomu ya Mbagala na Gongolamboto mwaka 2009 na 2011 ambayo yaligharimu maisha ya Watanzania wengi, na wengi kuachwa vilema. Nikukumbushe pia habari za machafuko ya Zanzibar na kuchomwa kwa makanisa Dar es Salaam.

Mheshimiwa Rais, hayo yote ni tisa; kumi ni suala la gesi ambalo hadi sasa tumejulishwa kuwa wamefariki watu saba na wengine kujeruhiwa. Vilevile huko Morogoro na kuna mapigano ya wakulima na wafugaji, na huko Kariakoo kuna machafuko ya Machinga na Migambo.

Yote haya yanatokea na wewe uko kimya, sijui kwa nini. Umeshakuwa utamaduni wako kukaa kimya pale mambo yaanzapo na hatimaye kuibuka mwishoni mambo yakiwa yameshaharibika. Sijajua vizuri ni nani wanakushauri kufanya hivyo, kukaa kimya, ila nikujulishe tu kuwa wakushaurio wanakushauri vibaya.

Mheshimiwa, hali ya nchi iko tete sana hadi sasa. Hili swala linahitaji hatua madhubuti, si za wasaidizi wako tena, si za Mawaziri wako tena, bali wewe mwenyewe. Kutokuridhishwa na utendaji wako kumeenea kila mahali. Watoto kwa wakubwa, wanawake kwa wanaume, wanalalamika; watu wameshindwa kujua nchi unaipeleka wapi. Kumekuwa na matumizi ya silaha kwa kiasi kikubwa sana. Hali inatisha.

Mheshimiwa Rais, cheche ndogo yaweza kuutafuna msitu mkubwa, hasa msitu wenye nyasi kavu. Tanzania imekabiliwa na matatizo mengi ya huduma za afya, elimu, umeme, barabara, kupanda kwa bei za vyakula, n.k. Kwa ujumla, haya yote yanaifanya Tanzania iwe kama msitu wenye nyasi kavu. Zinapotokea cheche za moto kila upande wa msitu huu, kwa hakika msitu huu utateketea. Msitu huu utakapoteketea, wewe ndiwe utakayeingia matatani zaidi. Kwa hakika, kilichowakuta wakina Ben Ali, Hussein Mubarak na wengine wengi, kinainyemelea nyumba yako.

Mheshimiwa Rais, najua walishakutahadharisha wengi, ila nami niongezee. Suala la Mtwara si la kunyamaziwa hivyo. Nakuhakikishia, badala ya kuvuna gesi Mtwara, utavuna damu, ikiwa hutachukua hatua za haraka. Watu wamechoshwa na unyonyaji wanaofanyiwa. Watu wameota sugu mioyoni mwao. Watu wameshindwa kusubiri, watu wanataka mabadiliko. Watu wanataka wasikilizwe, watu wanataka watambuliwe, watu wanataka waheshimiwe.

Mheshimiwa, ni kweli wewe una majeshi, una askari, una silaha. Lakini wananchi wana mioyo ya ujasiri, wana umoja, wana ndoto, wana hoja; hizo ndizo silaha zao ambazo kamwe majeshi na silaha haviwezi kuzishinda. Ndio maana hadi sasa watu wamekufa huko Mtwara. Watanzania wameshafikia hatua hiyo, wako tayari kufa kwa ajili ya haki. Na kama huchukui hatua za haraka za kutekeleza maoni ya Wananchi wa Mtwara, tegemea vifo vingi zaidi.

Waswahili walisema, mzarau mwiba mguuni huota tende. Naona unapuuzia huu mwiba. Tambua kuwa, mwiba unatakiwa uutoe mapema. Usipoutoa mapema, hakika, utaota tende, hakika utaozesha mguu mzima, na mwisho wake, utaupoteza mguu wako au hata mwili mzima. Kamwe, huwezi kukabiliana na madai ya wananchi kwa kuwaonyesha una majeshi makubwa kiasi gani; wala si kwa kuwaonyesha una silaha kiasi gani; wala si kwa kuwaonyesha wewe ni mwamba kiasi gani. Madai ya wananchi yanatakiwa yafafanuliwe kwa hoja na si vioja, kwa uongofu na si hofu, kwa utashi na si matusi. Watu wanapolia hadi machozi yanapowakauka, na bado wasione kusikika kwa vilio vyao, mwisho wanaamua kuzitoa damu zao, na hizo zitokapo hata wewe hutakuwa salama.

Mheshimiwa, migomo na maandamano vinapokuwa sehemu ya maisha ya wananchi, matatizo yao yasipotatuliwa hadi wagome na kuandamana, tunazalisha kizazi kikaidi, kisichoogopa silaha, kisichoogopa majeshi, kizazi kisichouogopa uongozi. Hya yakishatokea (na yameanza kutokea) nchi itaingia vitani, nchi itakuwa machafukoni, nchi haitatawalika. Tatua matatizo ya wananchi yangali machanga; udongo uwahi ungali maji. Juzi ilikuwa Arusha, leo ni Mtwara, kesho itakuwa Mwanza na Kigoma, keshokutwa Tanga na Pwani; mwisho itakuwa nchi nzima. Matokeo yake utatafuta pa kukimbilia wala hutapaona kamwe.

Tafadhali ipokee barua yangu.
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...