Sunday, March 3, 2013

Makachero wa kimataifa wabaini Tanzania ni kituo dawa za kulevya, Serikali yakiri!

Kwa wale ambao hamjasoma gazeti ala Mtanzania la leo J.pili kuna taarifa imenishitua kuhusu Taifa Letu Ebu ipitieni wandugu.

*Makachero wa kimataifa wabaini ni kituo dawa za kulevya
*Inapokea shehena ya zaidi ya dola bil 2 kila mwaka
*Wasichana wa Kitanzania watumika, Serikali yakiri

IMEBAINIKA kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi tatu kubwa duniani zinazotumika kama kituo cha usambazaji wa dawa za kulevya katika nchi za ukanda wa maziwa makuu na zile zilizoko kusini kwa jangwa la sahara.


Utafiti wa uliofanywa na taifa moja kubwa la Ulaya Magharibi, kuhusu biashara ya dawa za kulevya barani Afrika na gazeti hili kudokezwa, umethibitisha pasipo shaka kuwa nchi za Amerika ya Kusini na zile za Bara la Asia zinazojihusisha na uzalishaji na uuzaji dawa za kulevya, zimekuwa zikiitumia Tanzania kama kituo chake muhimu kusambaza dawa hizo sehemu mbalimbali duniani.


Kubainika kwa ukweli huo, kunathibitishwa na idadi kubwa ya makachero wa mataifa makubwa ya Magharibi waliopo nchini wanaoendesha uchunguzi wa siri wa mwenendo wa biashara ya dawa za kulevya na namna ambavyo Watanzania wanatumika kufanikisha biashara hiyo, kama wasafirishaji wakuu kwa nchi za jirani hususani zilizo kusini mwa Afrika.


Vyanzo mbalimbali vya habari vilivyofikiwa na Mtanzania Jumapili vimeeleza kuwa wafanyabiashara wakubwa wa mihadarati kutoka mataifa ya Bara la Asia yanayostawisha mimea inayozalisha aina ya dawa hizo, katika miaka ya karibuni wamekuwa wakitumia Pwani ya Tanzania kama kituo kikuu cha kusafirishia bidhaa zao.


Mataifa ambayo wafanyabiashara wake wamebainika kuitumia zaidi Pwani ya Tanzania katika biashara hiyo haramu ni Pakistani na Afghanistan ambayo yanafahamika zaidi kwa uzalishaji wa dawa za kulevya aina ya Heroin na Opium.


Mataifa mengine ni yale ya Amerika Kusini ya Columbia na Bolivia ambayo ni maarufu kwa uzalishaji wa Heroin ambayo pia yameigeuza Pwani ya Tanzania kuwa kituo chake kikuu cha usafirishaji dawa za kulevya.


Mtanzania Jumapili imedokezwa kuwa mawakala wa dawa za kulevya kutoka mataifa hayo wamekuwa wakisafirisha bidhaa zao kwa njia ya maji hadi karibu na Pwani ya Bahari ya Hindi kwa upande wa Tanzania Bara na kutia nanga kati kati ambako boti za wavuvi zimekuwa zikitumika kwenda kuchukua mzigo na kisha kuipitisha katika bandari bubu zaidi ya 30 zilizoko Pwani na Dar es Salaam na nyingine nyingi katika maeneo ya Tanga, Bagamoyo, Mtwara na Lindi.


Utafiti katika maeneo hayo ya bandari bubu umeonyesha kuwa mawakala wa dawa za kulevya husafirisha mizigo yao kwa njia ya maji hadi Zanzibar na Dar es Salaam.


Habari zaidi zinaeleza kuwa wakiishafikisha mizigo yao Zanzibar ambako wafanyabiashara za mihadarati kutoka sehemu mbalimbali duniani huinunua na kuisafirisha kwenda nchi za Ulaya Magharibi kwa kutumia ndege ndogo zinazotumika kubeba watalii ambako si rahisi kukamatwa.


Baadhi ya watu waliohojiwa na Mtanzania Jumapili kuhusu usafirishaji wa dawa hizo walieleza kuwa baada ya kufikishwa Zanzibar na kununuliwa na wafanyabiashara wakubwa, hukodisha ndege ndogo zinazotumiwa na watalii hususan wanaotoka Italia ambazo huruka moja kwa moja pasipo kusimama njiani. Usafiri huo unaaminika kuwa salama zaidi kwa kusafirisha dawa za kulevya kwa sababu ndege zinazotumika hazipiti kituo chochote na hivyo hazina ukaguzi wa kutosha.


Utafiti mwingine umeonyesha kuwa kama wauzaji wanataka kusafirisha mzigo kwenda sehemu nyingine wanawatumia wasichana wa Tanzania ambao wanasafirisha dawa za kulevya wakitokea Dar es Salaam kwenda nchini Afrika Kusini wakitumia usafiri wa basi.


Taarifa zinaonyesha kuwa wasichana hao hupakizwa dawa za kulevya tumboni na kusafiri kwa njia ya basi hadi mji mkuu wa Pretoria Afrika Kusini ambako baada ya kuupakua kwa njia ya haja kubwa, mzigo unaotakiwa kubaki Afrika Kusini utabaki na ule unaotakiwa kusafirishwa kwenda nchi nyingine taratibu nyingine hufanywa nchini humo.


Habari zaidi zinaeleza kuwa, ili kuondoa mashaka wasichana hao hulazimika kukaa nchini humo kwa kipindi cha miezi miwili hadi mitatu wakifanya biashara ya ukahaba ili kuondoa mashaka kwa vyombo vya ulinzi vya nchi hiyo kisha hurudi katika vituo vyao vya Dar es Salaam na Zanzibar ambako hupakizwa mzigo mwingine.


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi, ambaye ofisi yake inahusika na udhibiti wa dawa za kulevya alipoulizwa kuhusu habari hizi aliliomba gazeti hili limtafute Kamishna wa Tume ya Kuratibu Udhibiti wa dawa za kulevya Christopher Shekiondo.


Akizungumza na gazeti hili, Shekiondo alikiri Meli hizo kubwa kuleta madawa ya kulevya zikitokea katika nchi za Afghanistan na Pakistani lakini alisema hafahamu kuhusu makachero wa kimataifa kuendesha uchunguzi huo hapa nchini.


“Ni kweli katika harakati zetu za ukamataji tumegundua meli kubwa zimekuwa zikija hadi maeneo ya karibu na pwani katikati ya maji, ambako boti ndogondogo za wavuvi zimekuwa zikifuata na kuja kupitisha kwenye bandari bubu za Dar es Salaam, Bagamoyo, Lindi na Mtwara”


Alisema kiasi chote cha dawa za kulevya kinachozalishwa nchini Afghanistan asilimia zaidi ya 82 kinasafirishwa kwenda katika nchi za Iran, Pakistani na Tanzania.


Kamishna Shekiondo alipoulizwa ni kiasi gani cha dawa za kulevya kinaletwa na meli hizo, alisema si rahisi kufahamu lakini akasema ni kingi ukilinganisha na kile kinachopitishwa kwa njia ya kumeza.


“Wanaopitisha kwa meli ndio wanaoingiza kiasi kingi kama kilogramu 100-200 lakini wanaomeza wanaweza kumeza kama kilogramu moja kasoro” Alisema Shekiondo.


Kuhusu wasichana wa kitanzania kutumika, Shekiondo alikiri na kusema kuwa si Afrika Kusini tu bali hata katika maeneo mengine duniani.


Shekiondo alisema wapo wasichana wa kitanzania wengi tu katika magereza ya nchi mbalimbali duniani, huku akitolea mfano Brazil ambako kuna Watanzania takribani 100.


“Marekani, Argentina, Perue, China mpaka Japan na Australia Watanzania wako wengi tu huko wamekamatwa na sisi hapa tunaendelea kupata taarifa juzi tu tumekamata kilogramu 3, Lindi tulikamata kilo 81 za Cocaine, kilo 92 tulikamata Tanga” alisema


Alisema wanachofanya wao kwa sasa ni kuendelea na mchakato wa kupata taarifa zaidina kuwafahamu watu wanaoingiza dawa za kulevya ili waweze kuchukuliwa hatua na kukomesha biashara hiyo.

Source; JAMII FORUM 
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...